Mshambuliaji wa klabu ya Liverpool na timu ya taifa ya Ureno, Diogo Jota, amefariki dunia katika ajali ya gari akiwa na umri wa miaka 28. Ajali hiyo ya kusikitisha pia imemgharimu maisha kaka yake, André Silva, ambaye pia alikuwa mchezaji wa kandanda na mwenye umri wa miaka 26.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na BBC na Sky News, ajali hiyo ilitokea katika jimbo la Zamora, nchini Hispania, majira ya saa 6:30 usiku (saa za Hispania), siku ya Alhamisi, Julai 3. Polisi wa Kikosi cha Guardia Civil wamesema gari walilokuwa wakisafiria lilitoka barabarani na kulipuka moto, na wawili hao walikutwa tayari wamefariki dunia.
Shirikisho la Soka la Ureno (FPF) lilithibitisha vifo vyao kupitia taarifa rasmi likisema kuwa “limegubikwa na huzuni kubwa”, huku Liverpool FC nao wakitoa salamu za rambirambi kupitia picha ya Jota yenye rangi nyeusi na nyeupe kwenye ukurasa wao wa X (zamani Twitter), ikisindikizwa na maneno:
“Liverpool Football Club imehuzunishwa sana na kifo cha kusikitisha cha Diogo Jota.”
Klabu hiyo iliongeza:
“Tumejulishwa kuwa Jota mwenye umri wa miaka 28 amefariki baada ya ajali ya barabarani nchini Hispania akiwa na kaka yake, André. Tunawaomba watu wote waheshimu faragha ya familia, marafiki, wachezaji wenzake na wafanyakazi wa klabu katika kipindi hiki kigumu.”
Kifo cha Jota kimetokea siku chache tu baada ya kufunga ndoa na mpenzi wake wa muda mrefu, Rute Cardoso, tarehe 22 Juni 2025. Jota alishiriki video ya harusi yao kwenye Instagram saa chache tu kabla ya ajali hiyo kutokea, akiandika:
“Siku ambayo hatutaisahau kamwe 🤍.”
Mke wake naye alichapisha picha tarehe 28 Juni na kuandika kwa Kireno:
“22 Juni 2025 • Ndiyo kwa milele .”
Kwa sasa, polisi wanaendelea kuchunguza chanzo cha ajali, huku wakithibitisha kuwa hakukuwa na gari jingine lililohusika.
Katika ujumbe wa kuomboleza, Cristiano Ronaldo, ambaye ni mwenzake wa timu ya taifa, alieleza masikitiko yake kupitia Instagram:
“Hili halina maana yoyote… Tumekuwa pamoja hivi karibuni kwenye timu ya taifa, na sasa umeshaoa. Nawapa pole familia yako, mkeo na watoto wako. Najua utakuwa nao kila wakati. Pumzika kwa amani Diogo na André. Tutawakumbuka daima.”
Rais wa Shirikisho la Soka Ureno, Dr. Pedro Proença, alisema:
“Tumepoteza mabingwa wawili. Vifo vya Diogo na André Silva ni pigo lisilozibika kwa soka la Ureno. Tutahakikisha tunahifadhi urithi wao kila siku.”
Shirikisho pia limeomba UEFA kufanya dakika moja ya ukimya kabla ya mechi ya timu ya wanawake ya Ureno kwenye Euro ya Wanawake siku ya Alhamisi.
Diogo Jota alijiunga na Liverpool Septemba 2020 akitokea Wolverhampton Wanderers kwa ada ya dola milioni 54. Akiwa Liverpool, alishinda Premier League mwezi Mei 2025 na kuichezea timu ya taifa ya Ureno mara takribani 50, akifunga mabao 14.
Taarifa zaidi kutoka Liverpool FC kuhusu tukio hili bado hazijatolewa rasmi.